HATMA YA MAPINDUZI YA BOLIVARIA NCHINI VENEZUELA NA FUNZO LA MAPAMBANO ULIMWENGUNI

Na Joel Ntile

“Ninaweza kukosolewa na kulaumiwa kwa makosa mengi niliyoyafanya. Hata hivyo, kitu kimoja ambacho hawawezi kunilaumu ni juu ya uaminifu na uzalendo wangu kwa nchi yangu. Sitoweza (kamwe) kulaumiwa kwa kuwa nimeisaliti nchi yangu.”Ndugu Nikolas Maduro (Rais wa Venezuela)

Maduro

Taifa la Venezuela linapitia katika kipindi kigumu sana kutokana na makabiliano makubwa yanayoendelea kati ya serikali na upinzani nchini humo. Wakati upande wa serikali ukihusisha wafuasi na watetezi wa Mapinduzi ya Bolivaria, wakiongozwa na muungano wa chama cha kijamaa nchini humo (PSUV); nao upande wa upinzani unaongozwa na muungano wa vyama vya upinzani (MUD), unaoungwa mkono na serikali ya Marekani na washirika wake. Hali hiyo ya kutofautiana, baina ya makundi haya, imesababisha mapigano, maandamano na vurugu katika miji mbalimbali, hususani Carcas (mji mkuu), na vivyo hivyo kupelekea majeruhi na vifo vya baadhi ya raia wa nchi hiyo.

Chavez Maduro and Bolivar
Walio katika picha iliyoshikiliwa ni Hugo Chavez kushoto, Simon Bolivar katikati na Nikolas Maduro kulia

Makabaliano haya nchini Venezuela yanaonekana kudumu kwa takribani miongo miwili sasa, tangu kufanikiwa kwa mapinduzi ya Bolivaria mwaka 1999, yakiongozwa na Kamaradi Hugo Chaves pamoja na wenzake. Mapinduzi haya yalipewa jina la mpigania uhuru wa karne ya 19 katika nchi mbalimbali za Amerika ya Kusini, Kamaradi Simon Bolivar; ambapo yalitokea baada ya kudumu kwa muda mrefu mapambano ya wakulima na wafanyakazi wakipinga unyonyaji wa makampuni ya kibeberu, hususani yale yaliyokuwa yakijihusisha na biashara ya mafuta.

Kilele cha mapinduzi kilifika pale ambapo Hugo Chavez na viongozi wengine wa kijeshi walipokataa amri ya kuwashambulia wananchi waliokuwa wakiandamana. Hatua hii ilifuatiwa na wakaidi hawa kufanya jaribio la kuiangusha serikali; hata hivyo jaribio hili lilishindikana na kupelekea kikundi hicho kuwekwa kizuizini kwa miaka miwili kabla ya kuachiwa kutokana na shinikizo la wananchi. Na viongozi hawa walipotoka waliendeleza mapambano kupitia chama cha 5TH REPUBLIC MOVEMENT, ambapo walifanikiwa kuwang’oa vibaraka wa Ubeberu na Unyonyaji katika Uchaguzi Mkuu wa 1999.

Chavez 3

Ushindi wa uchaguzi mkuu hatimae ulisimika mafanikio ya Mapinduzi ya Bolivaria; ambapo kwaa mujibu wa Hugo Chavez na wenzake mapinduzi haya ni hatua ya mapambano ya wavujajasho ambapo msingi wake ni: Umajumuhi wa Amerika ya Latini; Ujamaa; Fikra za Utawala wa Watu Pamoja; na Upingaji Ubeberu na Mifumo Kandamizi Ulimwenguni kote.

Katika harakati za kuiishi misingi ya Mapinduzi ya Bolivaria, kama yalivyokuwa yakishadadiwa na Mwanamapinduzi Simon Bolivar, taifa la Venezuela lilifanikiwa kuandika Katiba Mpya iliyowapa mamlaka zaidi wananchi katika uamuzi na kujipangia mambo yao. Pamoja na mengine mengi, Serikali ya Venezuela ilitaifisha biashara ya uchimbaji wa mafuta na vivyo hivyo kuelekeza mapato yote yaliyopatikana katika biashara hiyo kugharamia huduma za afya, elimu na makazi ya wananchi. Na ni katika hatua hii, zaidi ya kaya maskini milioni mbili zilipatiwa makazi ya bei nafuu; mamilioni mwa watoto wa maskini waliweza kuendelea na masomo ya elimu ya juu; zaidi ya mashamba makubwa 1,200 yaliyokuwa yanamilikiwa na makampuni binafsi walipewa wananchi waendeshe shughuli za uzalishaji kupitia ushirika wa pamoja.

Kiujumla wake, Mapinduzi ya Bolivaria yalilenga katia kuimarisha utu na heshima ya wananchi wa Venezuela. Na ni kwa mafanikio haya ndio yaliyopelekea Kamaradi Hugo Chavez kusimama kidete katika kipindi chote cha uhai wake kuwa mtetezi mkubwa wa misingi ya Mapinduzi ya Bolivaria; na kuhakikisha serikali ya Venezuela, wakati wake, kuilinda miradi ya kijamii iliyozaliwa na mapinduzi hayo. Hatua na mwenendo ambao umerithiwa na mrithi wa Hugo Chavez, Ndugu Nikolas Maduro.

maduro_diosdado_chavez_efe

Kamaradi Nikolas Maduro tangu kuingia madarakani, (2013), amedhihirisha dhamira yake katika kuendeleza misingi ya Mapinduzi ya Bolivaria. Hata hivyo kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Hugo Chavez, Ndugu Nikolas Maduro amekuwa katika mapambano makali dhidi ya wapinzani wanaobeza hatua za serikali katika kutekeleza misingi ya Mapinduzi ya Bolivaria. Wapinzani hawa badala yake wamevitwaa vyeo vya kuwa mawakala na vipaza sauti wa sera za Ubepari.

Makabiliano ya Venezuela hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa mataifa ya Cuba na Bolivia waliochukua hatua ya kuanzisha jumuia mbadala ya ushirikiano baina ya nchi za Latini Amerika (katika kutekeleza dhana ya Umajumuhi wa Dunia, yamekuwa yakijikita katika itikadi baina ya msimamo wa serikali kuufuata mrengo wa kijamaa dhidi ya makundi ya kibepari, yanayodhaminiwa na taifa la Marekani. Hivyo wakati serikali ya Maduro, Castro na Morales wakiazimia kusimamia misingi ya maendeleo ya kweli… Trump, Mabwanyenye Uchwara katika nchi za Kilatini na taasisi za kibeberu wamekuwa wakiwashambulia waenezi hawa wa Ujamaa katika jitihada za kutetea maslahi yao (kundi la wachache dhidi ya wengi) na kuilinda mirija yao ya unyonyaji.

Chavez and Castro

Katika jitihada za kudhohofisha uenezi wa itikadi ya kijamaa, nchi na jamii za kibepari zimefanikiwa kuweka vikwazo vya mataifa yote yaliyokataa kuridhia kuwa sehemu ya uchumi wa kibepari. Na hali hii ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi ndio inayoitafuna, kama sio kuelekea kuitafuna taifa la Venezuela; ambapo sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu kama vile chakula na madawa ya binadamu (Rais Maduro nae imekiri juu ya upungufu huu). Na upungufu huu unaotokana na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni hasa dola ya Marekani, ambapo ni nchi ya Marekani inayoagiza asilimia 60% ya mafuta.

Ni ukweli usiopingika kuwa maamuzi ya Marekani kuiwekea vikwazo Venezuela hayatokukoma mpaka itakapotimiza lengo lake. Nalo lengo hilo ni wao (kama Marekani) kumiliki, kuhodhi na kunufaika na mafuta ya Venezuela. Hata hivyo azma yao hiyo haitafanikiwa mpaka pale watakapoizika serikali ya Maduro na vivyo kuzizika fikra za kijamaa. Na ni kwa mantiki hii Marekani itaendelea daima kuiandama nchi hiyo, sio tu kwa kutumia vita ya kiuchumi inayoiendesha tokea mwaka 1999 na kuonekana kutokufanikiwa, bali kwa hatua zaidi zenye lengo la kudhofisha hali ya ubinadamu na amani. Mbali zaidi, mpaka pale Marekani watakapofanikiwa kuwapenyeza vibaraka wao wa upinzani kushika nyadhifa za juu za uongozi.

Hata hivyo kama taifa, wananchi na viongozi wao hawajakaa nyuma na kimya pasipo kuzipinga dhulmati za Marekani na chokochoko za mabwanyenye uchwara. Wakati Maduro akiendelea mapambano ya moja kwa moja dhidi ya Trump na Marekani; jeshi la Venezuela limetangaza mshikamano na serikali; na mahakama ya nchini humo nayo imetangaza kuwa upande utu na kweli ambapo hiyo iliipokonya madaraka bunge la kibwanyenye na kulipa baraza la wananchi kufanya mabadiliko ya kikatiba. Baraza la wananchi linaundwa na wananchi wenyewe kupitia vyama vya wakulima, ushirika, wafanyakazi, ushirika na wanafunzi; na maamuzi ya mahakama yalitokana na msimamo kuwa baraza hilo lina nafasi kubwa na ndilo linalobeba matakwa ya umma na lenye uwezo wa kuwaunganisha wananchi na kuwakilisha mawazo yao.

Maduro 2

Na kama alivyokwisha kukiri Kamaradi Nikolas Maduro katika nukuu ya mwanzo kabisa, licha ya jitihada za dhati zinazofanya katika kuulinda na kuutetea Ujamaa ulimwenguni, bado kuna haja kubwa ya kujihoji, kujikosoa (kama wajamaa) ilimradi kuweza kujidhatiti na kuhimili hila zote za ubepari na mifumo kagandamizi duniani.

Miongoni mwa mengi, tunapaswa kujifunza na kuyatafakari upya mapambano yetu yanayotegemea uagizaji wa bidhaa za msingi kutoka nje ya nchi, pasipo kutilia mkazo uwezeshwaji wa wananchi kujitegemea katika kuzalisha bidhaa za msingi ili kuepukana na utegemezi toka nje. Ni wakati wa mataifa haya ya kijamaa kuangalia zaidi ndani badala ya kutilia msisitizo mkubwa katika biashara ya kuuza nje, kitu ambacho kilipelekea mtikisiko katika nchi ya Venezuela toka mwaka 2014 baada ya anguko la bei la mafuta duniani.

Pamoja na kuwepo haja ya kupinga rushwa na urasimu unaoshika kasi ndani ya serikali na chama; pia ipo haja ya kukosolewa kwa mfumo wa uongozi unaotumiwa nchini Venezuela, unaoratibiwa na kuhodhiwa na maofisa wakuu wa jeshi. Licha ya kuwepo watetezi wa mfumo huu kwa minajili ya kujihami kwa serikali ya nchi hiyo dhidi ya dhulmati na hujuma za maadui (vibaraka wa mabeberu)… bado sikubaliani hoja hizo kwa maana wanamapinduzi wenyewe walikwishapata funzo mwaka 2002 ya kuwa mapinduzi ni watu na siyo serikali.

Hugo-Chavez

Wapo watakaobeza hili, lakini sharti tufahamu kuwa unaweza ukaiangusha serikali lakini hautaweza kuangusha hisia za kimapinduzi katika mioyo ya watu. Na ni kwa imani hii hii kuwa mapinduzi yatakuwa salama zaidi kama yataendelea kuwekwa mikononi wa wavujajasho wenyewe ili wayalinde na kuyaendeleza. Mfano dhahiri ukiwa ule wa wakulima, wafanyakazi na wapenda maendeleo wa nchini Venezuela walivyosonga mbele, bila ya kuhofia risasi za wapinga mapinduzi mwaka 2002, baada ya jaribio la kuiangusha serikali ya kimapinduzi ya Hugo Chavez. Ni wananchi ndio walioweza kumrejesha Hugo Chavez madarakani baada ya kuondolewa ikulu kwa masaa 47 na wafanyabiashara wakiongozwa na Bwanyenye Pedro Carmona alieyeunda serikali ya mpito iliyodumu kwa saa 47 kabla ya kutimkia uhamishoni.

the_coup_was_overturned_by_the_people.jpg_1662275357
Hakika watu wa Venezuela wameamka.

Mapambano na magumu nchini Venezuela yanatoa taswira halisi ya mapambano ulimwenguni kote. Na mbali zaidi hali ya nchini humo inatia moyo na faraja kwa wavujajasho wa ulimwengu katika azma ya kuthamini zaidi utu na usawa kabla ya kitu chochote. Hivyo basi, sharti kama wapenda maendeleo na wajamaa kuendelea kupigania umajumuhi wa ulimwengu, kwani pasipo umajumuhi wa ulimwengu hakuna ujamaa utakaosimama imara katika kisehemu kdogo cha dunia. Na ni katika hali hiyo ndiyo tutaweza kuwashinda mabeberu Venezuela, Latini ya Amerika, Afrika na Duniani kote.

#AlutaContinua

Mawasiliano: wajamaatanzania@gmail.com

Advertisements
Categories:

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s